Search

Sunday, October 20, 2013

Brandts atwisha mzigo wachezaji Yanga

Kocha wa Yanga, Ernest Brandts amesema benchi la ufundi lilishamaliza kazi ya maandalizi ya mchezo leo wa watani wa jadi wa ligi kuu ya Bara, hivyo kazi imebakia kwa wachezaji wake kuifunga Simba kwenye Uwanja wa Taifa.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Brandts alisema wakiwa kambini Pemba amekiandaa vizuri kikosi chake na kazi imebakia kwa wachezaji wake kukamilisha mafunzo hayo uwanjani.

Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana kwa njia ya simu pia, nahodha wa Yanga Nadir Haroub 'Canavaro' ambaye leo atakuwa na kazi ya kumkaba mshambuliaji anayeongoza kwa magoli, Amisi Tambwe, alilipokea jukumu hilo la wachezaji na kuahidi ushindi.


"Mchezo utakuwa mgumu," alisema Canavaro, "lakini kiuchezaji naamini sisi tupo vizuri zaidi yao (Simba).

"Na hata ukitazama vikosi vyetu sisi timu yetu haijabadilika sana ukilinganisha na wao, tuna nafasi kubwa ya kushinda."

Simba leo inaikaribisha Yanga kwenye mchezo ambao kikosi cha Jangwani kinapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

Beki huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars na Zanzibar pia alisema lengo la Yanga ni kuifikia Simba kwa pointi kwenye msimamo wa ligi kuu. Simba ina pointi 18 na Yanga 15 baada ya zote kucheza michezo nane.

Yanga inapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa leo kutokana na uwezo waliouonyesha katika michezo ya hivi karibuni huku Simba ikionekana kuwa na mapungufu kwenye safu yake ya ulinzi na kuonekana wachezaji wake kuchoka kila muda unavyokwenda.

Hata hivyo kocha wa Simba Abdallah Kibadeni alisema kuwa wamefanyia kazi mapungufu ya timu yake hasa suala la kuchoka mapema.

Kibadeni alisema kuwa kambi yao ya Bamba Beach wameitumia kuondoa kasoro hizo kwenye kikosi chake.

Katika mchezo wa mwisho uliowakutanisha timu hizo, Yanga iliibuka na ushindi wa magoli 2-0.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment